Utapeli wa fedha mitandaoni ufike mwisho|techplatform©

 
kwa kirefu kuendelea kukithiri kwa vitendo vya utapeli wa fedha kwa njia ya simu na umma uliamini baada ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole pengine vitendo hivyo vingekoma. Lakini hali imekuwa tofauti, kwani taarifa za utapeli na wahalifu wa mitandaoni kupitia simu unazidi kukua na ni rai yetu kwa mamlaka za kiserikali zinazohusika zikiwamo kampuni za simu, zishirikiane kukomesha wizi huu. Katika habari hiyo tumeandika namna watu wanavyotapeliwa mitandaoni na wanaojifanya ni wafanyabiashara, hasa wanaonadi bidhaa zao kupitia mitandao ya kijamii kama Instagram, lakini wakishalipwa ndio mchezo umeishia hapo. Kwanza utakuwa ndio mwanzo na mwisho wa mawasiliano yenu na wakati mwingine hata ana block (kuzuia) usiweze kumfikia licha ya kwamba kabla hujamtumia fedha kupitia namba anayokupa, mnakuwa na mawasiliano mazuri. Pamoja na usajili wa laini za simu kupitia kitambulisho cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) bado watu wameendelea kupokea ujumbe mfupi (SMS) wa kuwataka watume hiyo fedha kutumia namba fulani na inatajwa. Mbali na utapeli huo, wapo wanaodiriki kupiga simu kabisa wakijifanya ni wafanyakazi wa kampuni fulani ya simu kwamba kuna fedha zimetumwa kimakosa, lakini mwisho wanaoingia kwenye mtego hujikuta wakitapeliwa fedha. Ripoti ya kitengo cha uchunguzi wa makosa ya mtandao, inaonyesha jumla ya matukio 4,000 yaliripotiwa polisi na kufanyiwa kazi, lakini ukweli ni kwamba matukio yanayoripotiwa pengine ni machache kuliko uhalisia mitaani. Lakini Watanzania waliposajili simu mwaka jana kwa kutumia kitambulisho cha Nida mojawapo ya faida iliyoelezwa ni kwamba ilikuwa ni kudhibiti uhalifu wa mtandaoni, ukiwamo wizi wa fedha, utapeli na hata magenge ya kihalifu. Julai 1, 2020, mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) alitoa tangazo akisisitiza mtu binafsi atasajili laini moja tu kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kupiga simu, kutuma meseji au kutumia data. Sasa tunajiuliza, matapeli hawa wa mtandaoni wanapata wapi nguvu hizi za kuzidi mamlaka zetu ambazo tunaamini ziko vizuri kitekinolojia, kiasi kwamba hadi leo matapeli na wezi wa mtandaoni kugeuza eneo hilo kama shamba la bibi. Tunachokisikia huko mitaani, ni kwamba mchezo huu una mkono wa baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa kampuni za simu ambao wameruhusu watu kusajili laini zaidi matapeli hao kwa kutumia kitambulisho kimoja cha Nida. Hapa ndipo penye tatizo, kwani huko kwingine tutazunguka mbuyu lakini ukweli ni kwamba mchawi wetu katika utapeli huu ni mawakala wanaosajili laini za simu kwa alama za vidole, kutumia vitambulisho vya watu ambao hata hawana taarifa. Mwisho wa siku inapotokea tukio la wizi au utapeli, likifuatiliwa inagundulika kitambulisho kimoja cha Nida cha mteja A na alama zake za vidole, zimetumika kusajili vitambulisho vya watu ambao hana nasaba nao na hawafahamu. Ni lazima sasa TCRA waunganishe nguvu wakishirikiana na wataalamu wa Tehama na kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano, kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa. Tusingependa kuwafundisha wataalamu wetu ndani ya TCRA, kampuni za simu na polisi wetu wa kitengo cha makosa ya kimtandao (Cyber Crime Unit) namna ya kukabiliana na wimbi hili, lakini ifike mahali tuseme imetosha. Siku zote tunasema Serikali ina maguvu, ikiamua jambo lolote inaweza.

Post a Comment

Previous Post Next Post