Fahamu Simu za Zuri: Uchambuzi wa simu za Zuri C41 na Zuri C52
Kuna brands nyingi sana za simu janja zinazojitaidi kuingia katika masoko mapya ya simu yanayokua kwa kasi kwa sasa: hii ikiwa ni pamoja na Afrika. Leo pata kufahamu simu za Zuri, na tutaziangalia Zuri C41 na Zuri C52
Historia fupi, Simu za Zuri zinatengenezwa wapi?
Jina la Zuri haraka haraka unaweza pata wazo ni kampuni ya hapa hapa Afrika Mashariki…lakini si hivyo. Simu za Zuri zinatengenezwa na kampuni ya Zuri ya Hong Kong, taifa huru ndani ya China.
Kupitia mtandao wao Zuri.hk inaonesha wanatengenezwa vitu vingi vya kielektroniki zaidi ya simu tuu. Hii ni pamoja na spiker, vifaa vya WiFi, taa za LED, TV za LED pamoja na tableti.
Na sasa wameanza kusambaza simu zao katika soko la Afrika Mashariki, kuongeza ushindani dhidi ya Tecno, Huawei na makampuni mengine yatengenezayo simu zenye uwezo mzuri kwa bei nafuu.
Ifahamu Zuri C41
- Inakuja na toleo la Android 5.1 Lollipop
- Ina kioo (display) ya inchi 4, (WVGA Display)
- Prosesa ya Quad core ikiwa na RAM ya 512 MB
- Diski uhifadhi wa GB 4 – ila unapata memori kadi ya bure ya GB 8 ndani ya boksi lake. Memori kadi hadi ya GB 32 inaweza tumika.
- Ina kuja na uwezo wa laini mbili
- Betri – kiwango cha mAh 1400
- Ni ndogo, ikiwa na uzito wa gramu 140
- Kamera ya selfi ya Megapixel 2, na kamera kuu ya megapixel 5.
Ndani ya boksi tulikuta kuna chaja – USB na kichwa chake, earphones, screen protector, na makava mawili (la kufunga/kufunika na la kawaida). Simu ya Zuri C41 inapatikana katika rangi nyeupe na nyeusi, na inauzika kwa bei ya Tsh 130,000/= kwa Dar es Salaam
Zuri C52
Simu ya Zuri C52 ni ya ubora wa juu kidogo zaidi ya Zuri C41. Kuanzia kwenye muonekano wake na ata sifa zake za ndani Zuri C52 ni toleo linalovutia na lenye muonekano wa kisasa zaidi.
Ubunifu mzuri umeenda katika utengenezaji wa ‘body’ lake, ambapo ukiishika utagundua malighafi za mpira zimetumika katika utengenezaji wa kasha (body) lake.
Sifa za undani
- Ina kioo cha inchi 5 – display ya teknolojia ya FWVGA IPS
- Inakamera mbili, megapixel 2 kwa ajili ya selfi na kamera kuu ikiwa ni ya megapixel 8
- Prosesa ya Cortex A7 Quad Core 1.3 Ghz ikija na RAM ya GB 1
- Diski uhifadhi wa GB 8 na huku ukipata memori kadi (SD Card) ya bure ya GB 8 ndani ya boksi.
- Nayo inakuja na toleo la Android 5.1 Lollipop
- Betri – mAh 2000
- Uzito gramu 157
Simu hii pia inakuja kwenye boksi ikiwa na vitu kama vile chaja, screen protector, na kava la simu la kufunika (flip cover). Na inapatikana kwa Tsh 210,000/= | Kes 9,400/= ila kutegemea na ulipo bei inaweza ikawa ata juu ya hapo kidogo.
Nilivyopenda:
Uingiaji wa Zuri Mobile katika soko la Afrika Mashariki utazidi kuleta ushindani kwa makampuni mengine yanauza simu za bei nafuu kama vile Tecno na Huawei. Hili litaongeza ubora na ata kuona bei za simu zikishuka kidogo. Je Zuri Mobile wataweza kutanua mabavu kwenye soko lililoshikiliwa sana na Tecno na Huawei??? Muda utatuonesha…
Zuri C41 ni simu nzuri kwa ajili ya mtu anayeitaji simu ya bajeti ya chini – ila nje ya hapo haina kipya sana. Ila Zuri 52 ndio simu nayaweza simu inavutia na ina utofauti mzuri, hasahasa kwenye muonekano – ubunifu uliofanyika katika kuifanya iwe ya kuvutia na inayokaa vizuri kiganjani.
Kwenye kamera bado kuna maboresho yanaitajika, ingawa kiwango cha megapixel ni cha kawaida inaonekana uwezo wa autofocus si mzuri sana…ila kwa bei ya simu hizi si jambo la kushangaza.
Upatikanaji – Inaonekana kwa sasa tayari simu za Zuri zinapatikana katika maduka jijini Dar es Salaam na Nairobi na inategemewa zinaweza zikawa tayari zishaanza patikana katika maeneo mengine.