Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC yawa ya kwanza nchini Tanzania kuzindua mfumo wa mawasiliano wenye kasi ya 5G, ilifanya hivyo jana tarehe 1 mwezi Septemba, mwaka 2022. Hafla ya uzinduzi huo ilifanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom kwa sasa, Hilda Bujiku alitangaza ujio wa mfumo huo, huku akiendelea kuhakikisha nafasi ya Vodacom katika kutoa huduma bora ya mtandao na mawasiliano kwa ujumla nchini Tanzania.
Hafla hio pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Nnauye, ambaye alitumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo serikali imekuwa na itaendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo katika sekta ya mawasiliano, huku pia akibainisha namna ambavyo uwepo wa kasi kubwa zaidi ya mtandao nchini utachochea maendeleo zaidi katika sekta mbaimbali kama kilimo, uzalishaji wa viwanda pamoja na sekta nyingine nyingi.
Tanzania inajiuunga katika nchi kadhaa barani Afrika ambazo tayari zimeanza kutumia mfumo wa mawasiliano wenye kasi ya 5G, ambao una nguvu takribani mara 40 ya mfumo wa 4G, huku Vodacom wakipanga kutengeneza vituo vya mawasiliano ya 5G mia mbili katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kufikia Novemba 2022.
Tukio jingine la kushangaza katika Uzinduzi wa mfumo wa mawasilianio wa 5G ni pamoja na Mh. Nape Nnauye kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania kupitia 2 way 3D Hologram, Teknolojia ambayo ni ya kwanza kutumika kwa Dunia nzima.